Matibabu ya
magonjwa mbalimbali yanahusisha matumizi ya dawa kama nyenzo muhimu katika
kufikia lengo la tiba stahiki.
Katika kutumia
dawa, kuna nyakati ambazo kunatokea maudhi ambayo yanakuwa kama kikwazo kwa
mtumiaji wa dawa husika kwa kutegemeana na tatizo lake la kiafya. Mifano ya
maudhi hayo ni kama vile kuwasha kwa ngozi, kuhisi kutapika au kichefuchefu,
kuvimbiwa (Constipation), kuhisi kama kuna vitu vinakwangua tumboni, kuvimba
mwili na maudhi mengine tofauti tofauti.
Lengo la kutoa
matibabu kwa mgonjwa siku zote ni kwa madhumuni ya kumsaidia mgonjwa. Utoaji wa
matibabu kimsingi unafuata taratibu za kiafya ambazo zinazingatia mambo mengi
ikiwa ni pamoja na kulinganisha faida endapo mgonjwa atatumia dawa husika,
hasara zinazoweza kujitokeza endapo mgonjwa hatotumia dawa husika na pia maudhi
yanayoweza kujitokeza endapo mgonjwa atatumia dawa. Mambo yote haya kwa pamoja
huzingatiwa katika kufanikisha matibabu ya mgonjwa na kumuwezesha kuirejesha
afya katika hali ya uimara zaidi.
Pamoja na
kuzingatiwa mambo hayo katika matibabu, jambo la kukumbuka ni kwamba maudhi
haya ya dawa hayatokei kwa kila mtu. Watu tofauti tofauti wanaweza kutumia dawa
ya aina moja lakini, mtu mmoja akapatwa na maudhi hayo na mwenzake akabaki bila
usumbufu wowote.
Ili kuweza
kuepukana na maudhi haya na hatimaye ukatumia dawa kwa urahisi na ukamaliza
dozi kwa ukamilifu wake, ni vyema kuzingatia mambo yafutayo:
Awali ya yote,
sehemu kubwa ya mgonjwa kuweza kupata matibabu sahihi kwa maana ya dawa ni
zoezi linalohitaji taarifa sahihi za mgonjwa zipatikane ambazo zinaelezea kwa
kina kuhusu chanzo cha tatizo/ugonjwa na hali nzima ya ugonjwa hadi hapo ambapo
amefikia hatua ya kuonana na mtaalamu wa afya/daktari. Pasipokuwepo na taarifa
za kujitosheleza kutoka kwa mgonjwa kutapelekea kuathiri aina ya matibabu na
dawa ambazo zitatolewa kwa mgonjwa. Hivyo ni jukumu lako kama mgonjwa/mteja
kutoa taarifa sahihi za tatizo lako ili uweze kupewa dawa sahihi na kuepukana
na maudhi yasiyo ya lazima.
Kuna maudhi ya
dawa ambayo husababishwa na mapungufu ya mgonjwa katika kuitumia dawa kwa
usahihi kulingana na maelekezo ya dawa yanavyotakikana, sababu yaweza kuwa ni
mgojwa kutopewa maelekezo sahihi au pengine kujisahau au kutozingatia maelekezo
yanayotolewa.
Mfano wa maudhi
ambayo yanaweza kujitokeza kwa kutotumia dawa kwa ufasaha ni kama vile kuhisi
tumbo kujaa au kuvimbiwa, tumbo kukwangua.
Kwa aina hii ya
maudhi, hutokea pindi mgonjwa anapokosea kutumia dawa kwa usahihi mfano dawa
jamii ya vidonge vya kuongeza damu pamoja na dawa za maumizu.
Ili kuepukana na
maudhi ya aina hiyo inashauriwa kutumia dawa za jamii hiyo (dawa za maumivu)
nyakati ambazo tayari mgonjwa ameshakula chakula (tumboni kuwe na chakula). Pia
kwa maudhi ya kuvimbiwa na kuhisi kichefu chefu baada ya kutumia dawa za
kuongeza damu, inashauriwa kutumia dawa hizo sambamba na vyakula au vinywaji ambavyo husaidia dawa
hizo kuyeyuka na kuingia katika mfumo wa damu kwa urahisi. Mfano wa vyakula na
vinywaji hivyo ni kama vile nyama, vyakula vyenye asili ya uchachu au juice za
matunda.
Pia kuna maudhi
ambayo yanatokea kwa mgonjwa ambayo hutokana na asili ya dawa yenyewe. Mfano
unaweza kuitumia dawa vizuri kwa maelekezo sahihi lakini bado maudhi kama vile
ngozi kuwasha na kuhisi usingizi bado ukapata maudhi hayo.