Articles

UPIMAJI WA MALARIA KATIKA MADUKA YA DAWA MUHIMU

on

SAMSUNG CAMERA PICTURES

VITENDANISHI VINAVYOTUMIKA KATIKA UPIMAJI WA MALARIA

Hali ya Malaria nchini imepungua katika kipindi cha muongo (Miaka kumi) mmoja baada ya kutekeleza afua za kudhibiti malaria pamoja na kutumia njia nyingine za afya. Maambukizi ya malaria yamepungua kutoka asilimia 18% mwaka 2007/8 hadi kufikia 9.5% mwaka 2011/12. Sambamba na hali hiyo, mpango mkakati wa kudhibiti malaria kwa mwaka 2014 – 2020 ni kutimiza lengo la kupunguza maambukizi ya malaria kutoka wastani wa asilimia 10% kitaifa mwaka 2012 hadi kufikia kiwango cha asilimia 5% mwaka 2016 na hatimaye chini ya asilimia 1% ifikapo mwaka 2020.

Kupungua huko  kwa maambukizi ya malaria kutawezeshwa na jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na wananchi pamoja na serikali kwa mfano, usambazaji wa vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu, matumizi ya dawa ya kujikinga na malaria kwa wamama wajawazito (SP – Sulphadoxine Pyrimethamine), pia utoaji wa elimu kwa jamii juu ya namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Wizara ya Afya maendeleo ya jamii jinsia wazeee na watoto kupitia mradi wa kudhibiti malaria nchini, NMCP, kwa kushirikiana na Baraza la Famasi Tanzania, wameanzisha mradi wa majaribio katika Mkoa wa Morogoro ambapo watoa dawa katika maduka ya Dawa Muhimu, ADDO wamepewa mafunzo maalumu ya upimaji wa Malaria na utoaji wa dawa na elimu ya kujikinga na malaria kwa wateja ambao watakuwa wanafika katika maduka yao kupata huduma. Huduma hii ya upimaji wa Malaria itapatikana katika Maduka ya Dawa Muhimu ambayo watoa dawa wake wamepewa mafunzo hayo maalumu ya kupima malaria kwa kutumia kipimo cha MRDT. Sambamba na upimaji wa malaria, pia watoa dawa wamefundishwa namna bora zaidi ya kutoa huduma kwa watoto wenye matatizo ya kuharisha pamoja na neumonia. Dawa aina ya Amoxycillin myeyuko itatolewa kupitia cheti cha daktari ili kuwasaidia watoto wenye nimonia na kwa watoto wenye matatizo ya kuharisha watoa dawa wamefundishwa namna ya kutoa dawa ya Zinc iliyofungashwa pamoja na ORS (Oral Rehydration Salt).

Kupitia upimaji wa Malaria katika Maduka ya Dawa Muhimu, itasaidia kupunguza matumizi ya dawa za malaria pale zisipohitajika, kwani mazoea ya watu wengi ni kufika katika Duka la Dawa na kununua dawa bila kuwa na uhakika kama homa aliyonayo ni Malaria. Pia  itamsaidia mteja kupunguza gharama zisizohitajika za matibabu na kuwawezesha wananchi walio mbali na vituo vya tiba kuweza kupata vipimo kabla ya kutumia dawa za malaria.

Siyo kila homa ni Malaria, pima kwanza kabla ya kufanya uamuzi wa kutumia dawa.

Chanzo: Tanzlife Company Limited

About Jackson Nyabusani

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *